• frank@frankpseth.com
 • +255 (0) 713 275 301
 • Ministry

  MBINU za KIVITA – I

  “1 Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; 2 nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake” (2 Samweli 17:1, 2).

  Kama kuna mbinu ya muhimu vitani ni KUMDHOOFISHA adui yako (kumnyang’anya silaha, kumfarakanisha na watu wake, kumwondolea msaada au mahitaji ya muhimu, n.k.) kabla ya vita au wakati wa vita. Kumbuka, adui yako naye hufanya vivyo hivyo kwako!

  Hadithi niliyokuletea hapa ni sehemu ya matukio yaliyotokea wakati Absalom, mwana wa Daudi, alipopindua ufalme wa baba yake Daudi! Kabla ya kuingia Ikulu, Absalom alifanya kampeni kwa mika takriban minne (4), kujiongezea umaarufu na kujipatia watu wa kusimama naye kuutwa ufalme. Absalom alijijengea NGUVU za kupambana kabla hajaanza vita.

  Ujue unavyojiandaa kivita na adui yako naye anajiandaa! Hata kama hujiandai kwa chochote, au huna habari kama kutakuwa na vita, bado adui yako anajinoa kupambana na wewe!

  Kwa wasomaji wa Biblia wanajua haya mambo yalitokea kama Bwana alivyosema kwamba “ataleta uovu juu ya nyumba ya Daudi” baada ya kumuua Uria na kumtwa mkewe, ambaye ndiye mama yake mfalme Suleiman, mfalme aliyetawala baada ya Daudi.

  Nikitudi katika mada hii, ukiona mambo ya aina hiyo (kudhoofishwa kiroho au kimwili kwa makusudi), yanatokea katika ngazi yako binafsi, familia, kanisani, kazini au mahali ambapo unajua kuna msaada wa kukutegemeza, uwe macho, inawezekana adui anakuvizia ili AKUPIGE baada ya kukuvunja NGUVU au kukuondolea MSAADA wa karibu.

  Kwa mfano, kama ulikuwa na uwezo wa kusimama kwenye maombi kwa angalau saa nzima kila siku na kusoma Neno angalau milango michache kwa siku bila shida, tena ukisikia raha ya kuendelea kusoma tu; sasa unajishangaa maombi yamekatika ghafla tu, huwezi tena kusoma Neno, ukigeuka huku unaanza kuona vita za ajabu ajabu zinaibuka kwenye familia (mke/mume, watoto, ndugu, n.k.) au wale ndugu wa KIROHO wanakua mbali na mawasliano na watu wako wa MUHIMU yanakatika tu bila maelezo ya kueleweka, jipange, hiyo ni dalili kwamba unawekwa kwenye KONA ili adui AKUCHAPE!

  Wakati mwingine, unaweza kujikuta unaingia kwenye VISHAWISHI ambavyo havikuwahi kukusumbua hapo mwanzo, kwa mfano: rushwa, madili ya pesa chafu, uzinzi, n.k. Ujue unaletewa SUMU ya kukuvunja nguvu za kiroho ili UDHOOFISHWE kabla ya KUCHAPWA na adui; Uwe makini!

  Unawezaje KUPATA uhakika kwamba kuna jambo lisilo la kawaida linaendelea kwenye kambi ya adui? Angalia mambo mawili, naam, yapo matatu:-

  i. Uwe makini na WALETA-HABARI (hao ndio waliomuokoa Daudi). Usibishane nao, hizo habari zao, hata kama ni UMBEA, wewe zifanye PRAYER – POINTS!

  ii. Uwe makini na DHAMIRI yako (Amani ya Kristo na iamue mioyoni mwenu). Ukikosa amani, hiyo ni RED light, usinyanyue mguu hapo, la sivyo utachapwa!).

  iii. Uwe makini na Neno linalojirudia-rudia ‘msimu huo’, iwe ni redioni, mtandaoni, kanisani, n.k. Neno huja kama mvua iinyeshayo nchi; Mvua haiji wakati usio wa Msimu! Uwe makini na ‘Neno la msimu’, litakuja kwa namna ya tofauti na utaweza kujua tofauti ya ‘mvua za Masika’ na ‘manyunyu ya Kipupwe’; Msisitizo MOYONI mwako ni tofauti. Neno la Msimu linapenya kwa namna tofauti, utajua tu!

  Neema na Baraka za Mungu wetu ziwe kwako tangu sasa na hata milele. AMEN!

  Dr. Frank P. SethComments